Ijumaa, 10 Juni 2016
Zoezi La Usajili Vitambulisho Vya Taifa Kukamilika Desemba 31 Mwaka Huu Nchi Nzima
Mamlaka ya usajili wa vitambulisho vya Taifa Nchini Tanzania (NIDA) wametangaza kuwa ifikapo tarehe 31 mwezi 12 mwaka huu usajili wa vitambulisho utakuwa umekamilika nchi nzima. Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es salaam Bi.Rose Mdami, alisema "usajili utakamilika ifikapo tarehe 31 mwezi 12 mwaka huu Nchi zima na wananchi kuanza kutumia namba ya utambulisho kupata huduma" Bi.Rose Mdami ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hatiwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) aliwasisitiza Wananchi wote Nchini kuweza kujiandikisha mapema ili kuepuka usumbufu baadae. Pia Bi. Rose Mdami, amesema NIDA imepanga kutumia taarifa za NEC kukamilisha usajili wa awali na kutoa namba ya utambulisho kwa wananchi wote ambao hawakusajiliwa katika mfumo wa NIDA. Pia akifafanua, Bi.Rose amesema baada ya kuhakikisha kila mwananchi ana nambari ya Utambulisho.kila mwananchi atalazimika kukamilisha usajili wake ikiwa ni hatua ya kujaza vipengele vya maswali vilivyobakia katika fomu ya maombi ya vitambulisho kabla ya kupata utambulisho kamili. "Kama mnavyofahamu, katika usajili wa NEC fomu ilikuwa na vipengele 32 vya kujaza kulinganisha na fomu ya NIDA ambayo ina vipengele 74, hivyo ni lazima kila mwananchi kutambua, ili kuwa na utambulisho kamili lazima kujaza vipengele vilivyobaki pamoja na kuambatanisha nakala ya viambata vyake muhimu kuthibitisha taarifa za umri, uraia na makazi" alilisitiza.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni